Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Abdulmahdi Karbalai, mwakilishi wa Ayatullah Sayyid Ali Hussein Sistani, katika hotuba yake wakati wa hafla ya uzinduzi wa hatua ya kwanza ya ensaiklopidia “Jawahir al-Saghah fi Jam‘i Shuruh Nahj al-Balagha”, alisisitiza kwamba Nahj al-Balagha si kitabu cha fasaha na balagha pekee, bali ni ensaiklopidia kamili ya maarifa ya Kiislamu na kibinadamu, yenye mizizi katika Qur’ani Tukufu, mwenendo wa Mtume Mtukufu (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake) na mwenendo wa Amiri wa Waumini Imam Ali (amani iwe juu yake).
Sheikh Karbalai alisema katika hafla hiyo: Kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Baqiyyatullah al-A‘zam Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) kunahitaji mwanadamu kujitahidi kwa vitendo kumsaidia Imam huyo katika kipindi cha ghaiba; kwa sababu nusura ya Imam haikomei katika zama za kudhihiri kwake pekee, bali huanza kwa kushikamana na mafundisho na misingi ambayo Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao) wameisisitiza.
Aidha, alibainisha kwamba; Nahju al-Balagha si kitabu cha taaluma ya balagha pekee, bali ni chanzo cha maarifa chenye nyanja nyingi ambacho bado hakijapewa nafasi pana inayostahili katika miduara ya kielimu.
Mwakilishi wa Ayatullah Sistani aliongeza kuwa; Taasisi ya Sayansi za Nahj al-Balagha ina jukumu kubwa la kufafanua na kueleza maandiko ya kazi hii, hasa katika nyanja za Qur’ani, fikra, hikma na uongozi. Umuhimu wa utafiti huu wa kielimu upo katika kukusanya sharh zote katika mkusanyo mmoja na kuongeza uchambuzi, ulinganisho, pamoja na kuangazia kwa kina vipengele vya kiisimu na balagha vya maandiko ya Nahju al-Balagha.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa, ensaiklopidia “Jawahir al-Saghah fi Jam‘i Shuruh Nahj al-Balagha” inachukuliwa kuwa mradi mkubwa zaidi wa kielimu katika kukusanya, kuchambua na kulinganisha sharh za Nahj al-Balagha, na lengo lake ni kufufua elimu za kitabu hiki cha milele na kuthibitisha nafasi yake katika fikra na akili za jamii.
Ensaiklopidia hii ni mradi wa kielimu unaotekelezwa chini ya usimamizi wa Taasisi ya Sayansi za Nahj al-Balagha, iliyo chini ya Ataba Tukufu ya Husseini.
Maoni yako